HAKI ZA KIDIJITALI SI ANASA BALI NI MSINGI WA UCHAGUZI HURU NA WA HAKI.

 Imeandaliwa na Jeremia emanuel (futureMEDIAUpdate);

     Katika enzi hii ya kidijitali, uhuru wa mitandao na haki za kidigitali ni mihimili muhimu inayochochea maendeleo ya demokrasia, uhuru wa kujieleza, na ushiriki wa wananchi katika mijadala ya kitaifa. Hata hivyo, tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2025, hali ya mambo inaonyesha mwenendo wa kutisha wa kukandamizwa kwa haki hizi na serikali mbalimbali barani Afrika, ikiwemo Tanzania. Makala hii inachambua hali halisi ya haki za kidigitali na uhuru wa mitandao, namna zinavyokiukwa, athari zake kwa demokrasia, na wito wa kuchukua hatua za haraka kabla haijawa too late.



1. Haki za Kidigitali ni Nini?

Haki za kidigitali ni upanuzi wa haki za binadamu za msingi – kama vile uhuru wa kujieleza, faragha, na kupata taarifa – katika mazingira ya kidijitali. Hizi zinahusisha uhuru wa kutumia mitandao ya kijamii, kulinda taarifa binafsi mtandaoni, na kuunganishwa na intaneti bila bughudha wala vizuizi visivyo na msingi wa kisheria.#JamiiForums 

Katika uchaguzi wowote wa kidemokrasia, haki hizi ni muhimu kwa sababu huwezesha:

• Wananchi kupata taarifa kwa wakati.

• Vyombo vya habari kuripoti kwa uhuru.

• Wagombea kujieleza na kueleza sera zao kwa uwazi.

• Raia kutoa maoni na kujadili mustakabali wa taifa.

2. Namna Serikali Zinavyokandamiza Uhuru Huu

 Serikali zimekuwa zikitekeleza mbinu mbalimbali za kukandamiza uhuru wa mitandao kwa kisingizio cha "kulinda amani" au "kuzuia habari potofu." Zifuatazo ni baadhi ya mbinu hizo:

a) Kufungia au Kudhibiti Mitandao ya Kijamii

Wakati wa uchaguzi uliopita (2020), Tanzania ilishuhudia kufungiwa kwa mitandao kama Twitter, WhatsApp na Facebook. Watu walilazimika kutumia VPN ili kuwasiliana. Hii ni kinyume na haki ya kupata taarifa na uhuru wa mawasiliano.#uchaguzimkuu2025

b) Sheria Kandamizi kama ile ya Makosa ya Mtandao (Cybercrimes Act)

Sheria hizi zimekuwa zikitumika kama silaha ya kukandamiza wakosoaji wa serikali. Kwa mfano, mtu anaweza kukamatwa kwa kusambaza "taarifa za uongo" bila kuelezwa viwango vya ukweli na uongo vinaainishwaje kisheria.

c) Udhibiti wa Maudhui kwa Wachapishaji wa Mtandaoni

Wamiliki wa blogu na tovuti wanatakiwa kujisajili na kulipa ada kubwa ili kuchapisha habari. Hili linaweka vikwazo kwa uhuru wa vyombo vya habari na watetezi wa haki.

d) Ufuatiliaji Haramu wa Mawasiliano ya Raia

Serikali zimekuwa zikinunua vifaa vya ujasusi wa kielektroniki kufuatilia mawasiliano ya raia bila kibali cha mahakama. Hili linakiuka haki ya faragha na linazua hofu miongoni mwa watumiaji wa mitandao.

3. Athari kwa Demokrasia

Kandamizaji huu una madhara makubwa kwa uchaguzi huru na wa haki:

• Uoga miongoni mwa wapiga kura: Wananchi huogopa kushiriki mijadala ya kisiasa kwa hofu ya kufuatiliwa au kukamatwa.

• Kupungua kwa uwazi: Kukosekana kwa taarifa hurahisisha propaganda na taarifa potofu kutoka kwa mamlaka.

• Kunyamazisha wapinzani: Mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa la upinzani kueleza sera zao. Kufungiwa kwa mitandao ni sawa na kuwafunga midomo.

4. Upinzani wa Raia na Mashirika ya Kiraia

Mashirika ya kiraia, wanaharakati wa haki za kidigitali, na baadhi ya vyombo vya habari huru wameendelea kupaza sauti:

• Wanatoa taarifa za ukiukwaji wa haki.

• Wanahamasisha matumizi ya teknolojia mbadala kama VPNs.

• Wanashinikiza marekebisho ya sheria kandamizi.

Lakini juhudi hizi hukumbana na vitisho, vitendo vya ukamataji kiholela, na kunyimwa usajili au fedha za ufadhili.

5. Nini kifanyike kabla ya 2025?

Ili kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa huru, haki za kidigitali lazima zilindwe. Hatua muhimu ni:

a) Marekebisho ya Sheria Kandamizi

Bunge lifanye marekebisho ya sheria kama ya Makosa ya Mtandao, na kuweka masharti yanayozingatia haki za binadamu.

b) Uwazi wa Serikali kuhusu Udhibiti wa Mitandao

Kabla ya kuchukua hatua kama kufungia mitandao, serikali iwajibike kutoa sababu wazi, za kisheria, na zinazokubalika kimataifa.

c) Uwezeshaji wa Elimu ya Kidigitali kwa Umma

Wananchi wafundishwe haki zao za kidigitali na namna ya kuzilinda – ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia salama.

d) Ushirikiano wa Kimataifa na Mashirika ya Haki za Binadamu

Mashirika ya kimataifa kama Human Rights Watch, Amnesty International na UNDP yanapaswa kuweka presha kwa serikali za Kiafrika kuhakikisha uhuru wa dijitali unalindwa.

                 Hitimisho

Tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2025, uhuru wa mitandao na haki za kidigitali ziko katika hatihati kubwa. Huu si wakati wa kunyamaza, bali ni wa kupaza sauti kwa pamoja. Teknolojia ni chombo cha ukombozi, si kifaa cha ukandamizaji. Serikali zinalo jukumu la kulinda, si kuvunja, haki hizi. Na raia wanao wajibu wa kuzilinda kwa kuzijua, kuzidai, na kuzipigania.


“Uhuru wa mitandao si zawadi – ni haki ya msingi ya kidemokrasia. Tukinyamaza leo, kesho tutapigwa bila njia ya kuomba msaada.”






Comments

Anonymous said…
Wwo