KI AZIZI AFUNGUKA YEYE KUONDOKA YANGA AACHA UJUMBE MZITO
✍ STEPHANIE AZIZ KI AMEANDIKA
"Yeyote aliyewahi kusema kuwa kuaga kunauma… alikuwa anajua haswa alichokuwa anakizungumza.
Moyo wangu ni mzito ninapowashirikisha rasmi taarifa za kuondoka kwangu katika klabu ya moyo wangu, Yanga SC. Hii siyo tu kuondoka kwenye klabu – ni kuaga nyumbani, kuagana na familia, na kufunga sura muhimu sana ya maisha yangu iliyonilea na kunijenga kama mchezaji na kama mwanaume. Yanga ilinipa kusudi. Yanga ilinipa makazi ya pili, na hata mke wangu mzuri nimepata kupitia Yanga!
Nilikuja nikiwa na ndoto, lakini ninaondoka na kumbukumbu za maisha. Pamoja tumefanikisha makubwa – tumenyanyua makombe, tumetawala Afrika, tumeandika upya historia ya klabu, na kuwafanya mashabiki wajivunie kuvaa kijani na njano. Tulisimama kifua mbele kwenye nyakati nzuri, na tukashikamana katika vipindi vigumu. Lakini daima, kitu kimoja hakikuwahi kubadilika – roho yetu.
DAIMA MBELE NYUMA MWIKO siyo tu kauli ya mdomoni – haya ni maneno yaliyotubeba, yaliyotufunga pamoja, na kutukumbusha kuwa sisi ni mashujaa, tulioumbwa kwa ajili ya ubora. Nimeichukua roho hii ndani yangu, na popote nitakapokwenda, itaniongoza. Huu ni mtazamo wa ushindi, wa kutokata tamaa, wa kusonga mbele kila wakati – sasa ni sehemu ya maisha yangu milele.
Kwa MR. GSM, nguzo yetu pendwa, Kwa kaka yangu Anthony Mavunde, asante kwa kila kitu, Kwa Mhandisi Hersi, Rais wetu mchapakazi,
Kwa kocha wangu, benchi la ufundi lote, wachezaji wenzangu uwanjani, na zaidi ya wote – kwa mashabiki wetu wa kipekee: Asanteni sana kwa upendo na mchango wenu mkubwa.
Mmenishangilia, mmeniunga mkono, mmekuwa sehemu ya familia yangu. Sitasahau nyimbo zenu, shangwe, na mafuriko ya mashabiki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kila tulipocheza. Nawahifadhi nyote ndani ya moyo wangu.
Hii siyo mwisho. Bali ni mwanzo mpya. Yanga itaendelea kuwa sehemu ya mimi. Sehemu ya hadithi yangu. Sehemu ya roho yangu.
Mpaka tukutane tena... Daima Mbele, Nyuma Mwiko.
#Futuremediaupdate
Comments