UONGOZI WA CHUO KIKUU JORDAN UNIVERSITY COLLEGE (JUCO) WAKUTANA NA WANAFUNZI LEO : CHANGAMOTO ZA ICT, ADA NA USHIRIKI WA MATUKIO ZAJADILIWA KWA KINA
Katika kikao kilichofanyika leo kati ya uongozi wa Chuo kikuu Jordan university (JUCO) na wanafunzi, wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali na kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kitaaluma na kijamii ndani ya chuo.
Miongoni mwa waliojitokeza kuwasilisha changamoto kubwa ni Mwakilishi wa Tatu (CR) wa mwaka wa tatu Tito Khamis Katisha, pamoja na CR wa mwaka wa kwanza, Allen Msyete, ambao kwa pamoja walielekeza lawama zao kwa Ofisi ya TEHAMA (ICT) kuhusu huduma na mfumo wa kiteknolojia usioridhisha unaowakwamisha wanafunzi katika shughuli za masomo.
Aidha, wanafunzi wengine pia waliongeza sauti zao kwa kueleza matatizo yanayowakumba, ikiwemo ucheleweshaji wa huduma muhimu kutoka kwenye idara mbalimbali za chuoni.
Katika majibu yake, Mkuu wa Chuo aliwataka wanafunzi kushiriki kikamilifu katika matukio ya ndani ya chuo, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika maendeleo ya kitaaluma na kijamii.
Vilevile, suala la ada na ucheleweshaji wa boom liliibuka kwa nguvu, ambapo wanafunzi walilalamikia ucheleweshaji huo kuwa unawagharimu na kuwakwaza katika kutimiza masharti ya kifedha ya chuo. Wanafunzi wengi walionesha wasiwasi kutokana na deadline ya mwisho wa kulipa ada kuwa tarehe 30 Mei.
Ofisi ya DPAA (Mipango na Fedha) ilitoa ufafanuzi kuwa watazingatia hali za wanafunzi wote walioathirika na ucheleweshaji wa boom, na kuahidi kuwa kuna utaratibu utawekwa kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeathirika kwa namna ya kunyimwa haki yake ya kuendelea na masomo kwa sababu ya ucheleweshaji huo.
Kikao hicho kimeacha taswira ya mawasiliano ya wazi kati ya uongozi na wanafunzi, huku matumaini yakiwekwa kuwa hoja zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi kwa haraka na kwa maslahi ya wanafunzi wote.
na;jey future tz
Comments