AZIZ KI YUPO WYDAD KWA MKATABA WA MWEZI MMOJA


 

Vyanzo maalum vya habari kutoka ndani ya Wydad Casablanca vimeiarifu Radio Mars kwamba mkataba wa mchezaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephanie Aziz Ki na Wydad ni wa mwezi mmoja, huku kukiwa na kipengele cha kusaini mkataba wa kudumu wa miaka mitatu iwapo benchi la ufundi watashawishika na kiwango cha mchezaji huyo.


Kocha wa Wydad, Mohamed Amine Benhachem amethibitisha kwamba Klabu hiyo imeanza kutumia mifumo hiyo ya mikataba ikiwa ni sehemu ya mbinu ya majaribio inayolenga kupima ufaafu wa wachezaji wa kigeni kwa mtindo na mahitaji ya timu.

Benhachem alisema katika taarifa yake kuhusu programu waliyoitoa kupitia Al-Marikh Sports: 

"Mchezaji yeyote ambaye tutamsajili kwa mwezi mmoja na ambaye anaonyesha sifa za kiufundi na za kuridhisha, tutafanya chaguo la kumsajili rasmi kwa miaka mitatu."

Kwa upande wake, mwandishi wa habari Adel Al-Amari, mtangazaji wa kipindi cha "Al-Haqiqa fi 90 Minutes," alieleza kuwa hatua hii inawakilisha mkakati wa makusudi wa uongozi wa Wydad kulinda maslahi ya klabu.

Aliongeza, "Hali ya mchezaji Aziz K iko wazi. Klabu yake ya zamani ya Yanga ilipokea kiasi dola 100,000 kwaajili ya kumuachia nyota huyo na ikiwa atafanya vizuri wakati wa ushiriki wake katika Kombe la Dunia la ngazi ya Klabu, zoezi la kununua mkataba wake litaanzishwa."

CHANZO: RADIO MARS KUTOKA MOROCCO.

Comments