WANAFUNZI MBALIMBALI WAPIMA NGUVU ZA WAGOMBEA URAIS (JUCo)
Morogoro, Juni 1, 2025 – Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali ya wanafunzi wa Jordan University College (JUCo) unaotarajiwa kufanyika Ijumaa, tarehe 6 Juni, wanafunzi wameonekana kushika kasi katika mijadala ya kisiasa huku wakitathmini uwezo na sera za wagombea wa nafasi ya urais wa serikali ya wanafunzi.
Asubuhi ya leo, baadhi ya wanafunzi walizungumza na Future media kuhusu matarajio yao kwa uchaguzi huu. Wengi walieleza maoni tofauti kuhusu wagombea wakuu wanaowania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa wanafunzi.
Daniel Augustine, ametajwa na wengi kama kiongozi mwenye maono na mwelekeo wa mabadiliko chanya katika maisha ya kitaaluma na kijamii ya wanafunzi. Anaungwa mkono na kundi kubwa la wanafunzi wanaotamani uwazi, uwajibikaji, na usawa katika utawala.
Kwa upande mwingine, Abui Mkumbo anatajwa kuwa na mvuto mkubwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili, hasa kutokana na umahiri wake katika kujieleza na uwezo wa kusikiliza matatizo ya wanafunzi wa kawaida.
BAHATI APOLINATORY, anayeungwa mkono na baadhi ya viongozi wa mihadhara ya ndani, ameonekana kuwa na mtazamo wa kujenga mifumo ya kudumu ya usaidizi wa wanafunzi kielimu na kiutawala.
VICTA KAJORO, ambaye kwa sasa anashika kasi kwa upande wa kampeni mtandaoni, amejijengea jina kupitia shughuli mbalimbali za kijamii na za kujitolea, akisisitiza haja ya kushirikisha makundi yote ya wanafunzi bila ubaguzi.
Wanafunzi wengi wameeleza kuwa uchaguzi huu ni nafasi ya kipekee ya kuleta sauti ya mabadiliko na kuimarisha ustawi wa wanafunzi wote wa JUCo. Pia, wameeleza matumaini yao ya kuwa uchaguzi huo utaendeshwa kwa amani, haki, na uwazi.
Uchaguzi wa mwaka huu umeongeza msisimko chuoni, huku midahalo ikitarajiwa kuendelea hadi siku ya mwisho ya kampeni. Hali ya hewa ya kisiasa ndani ya chuo imejaa matumaini na mashaka, lakini wanafunzi wanaonekana kuwa tayari kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa busara.
Imeandaliwa na jey future tz
Comments