RONALDO AZIMA NDOTO ZA YAMAL KUTWAA BALLON D’OR

     Katika fainali ya UEFA Nations League 2025 iliyopigwa katika Uwanja wa Allianz Arena, Munich, ndoto ya kinda mahiri wa Hispania, Lamine Yamal, ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or imepata pigo kubwa baada ya Ureno kuibuka mabingwa kwa kuifunga Hispania kwa mikwaju ya penalti 5–3, kufuatia sare ya mabao 2–2 ndani ya dakika 120 za ushindani mkali.

Mchezo huo uliokuwa wa kiwango cha juu ulianza kwa kasi, Hispania wakitangulia kufunga kupitia kwa Martín Zubimendi dakika ya 21. Ureno walirejea kwa bao kali kutoka kwa Nuno Mendes dakika ya 26, kabla ya Mikel Oyarzabal kuiweka Hispania mbele tena kabla ya mapumziko. Kipindi cha pili kilimshuhudia Cristiano Ronaldo, nahodha wa Ureno mwenye umri wa miaka 40, akifunga bao muhimu dakika ya 61 na kuisawazisha mechi.

Katika mikwaju ya penalti, nyota wa Ureno Diogo Costa aliibuka shujaa kwa kuokoa mkwaju wa Álvaro Morata, huku Rúben Neves akiifungia penalti ya ushindi iliyohitimisha ndoto ya Hispania kutwaa taji la pili mfululizo.

Huku nyota kama Ronaldo na João Félix waking’ara, macho mengi yalikuwa kwa Lamine Yamal, kijana wa miaka 17 ambaye kwa miezi kadhaa amekuwa akitajwa kama mgombea mkubwa wa tuzo ya Ballon d’Or 2025, kutokana na kiwango chake bora katika klabu na timu ya taifa. Hata hivyo, kushindwa kutwaa taji hili kubwa kimataifa huenda kukampunguzia nafasi hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa Ronaldo ameibuka tena kuwa miongoni mwa waliovuta hisia na heshima ya kimataifa.

Kocha wa Ureno alimsifu Ronaldo kwa mchango wake mkubwa akisema, “Kila anapoingia uwanjani, anabadilisha mchezo. Alifunga bao muhimu, akawaongoza vijana wetu, na bado ana njaa ya ushindi.”

Kwa upande wa Hispania, kocha na wachezaji walikiri kupoteza nafasi muhimu, huku wengi wakimtia moyo Yamal kwa kusema bado ana muda mwingi mbele yake kufanya makubwa zaidi.

Japo fainali hii haikufungua mlango wa tuzo kwa Yamal, bado haijafunga kabisa — lakini kwa sasa, historia imeandikwa tena na mzee wa kazi: Cristiano Ronaldo.

#FUTURE MEDIA UPDATE 

#jeyfuturetz 

Comments