TISHIO LA SUMU KWA LISSU.CHADEMA YATAKA UCHUNGUZI HURU NA KAULI RASMI YA SERIKALI
Dar es Salaam, Julai 2, 2025 — Wasiwasi umeibuka miongoni mwa wananchi na jamii ya kimataifa kufuatia taarifa zinazodai kuwepo kwa mpango wa kumtilia sumu kiongozi wa kisiasa Tundu Lissu akiwa mahabusu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa usiku wa Julai 2, 2025, kutoka kwa vyanzo kadhaa huru, ikiwemo ujumbe wa Mhe. David McAllister — Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya — kumekuwa na madai ya njama ya kuua kwa sumu mhusika huyo wa kisiasa. Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii X (zamani Twitter), McAllister ameandika:
“Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za kutisha za jaribio la kumtilia sumu kiongozi wa upinzani wa Tanzania Tundu Lissu akiwa kizuizini.”
Taarifa hizi zimezusha hisia mseto miongoni mwa wananchi, wanaharakati wa haki za binadamu, na baadhi ya mabalozi wanaofuatilia kwa karibu mwenendo wa kisiasa na haki za kiraia nchini.
Kwa sasa, hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa vyombo vya dola au taasisi huru za uchunguzi kuhusu ukweli wa madai haya. Hata hivyo, wadau mbalimbali wamesisitiza umuhimu wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kuhakikisha uchunguzi huru na wa kina unafanyika, sambamba na kuhakikisha haki na usalama wa mtuhumiwa huyu anayedaiwa kuwa kwenye mazingira ya hatari.
Tukio hili limeibuka wakati ambapo kuna mjadala mkubwa nchini kuhusu uhuru wa kisiasa, haki za watuhumiwa, na nafasi ya vyombo vya dola katika kusimamia haki kwa usawa bila kujali itikadi au nafasi ya mtu katika jamii.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na haki za binadamu wanatoa rai kwa mamlaka husika — ikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Polisi na Magereza — kuhakikisha ulinzi wa watuhumiwa wote walioko kizuizini, sambamba na uwazi wa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya uchunguzi huu.
Comments